HATIMAYE mgogoro uliodumu kwa siku takriban mbili mpakani mwa Tanzania na Zambia umemalizika huku serikali ya Tanzania ikiwaonya jirani zao hao kutorudia tena vitendo vya kuwanyanyasa raia wake.

Mgogoro huo ambao ulisababisha kujeruhiwa kwa watu kadhaa wa pande zote mbili sanjari na hasara ya mamilioni ya fedha, ulimalizika baada ya mkutano baina ya wawakilishi wa serikali za pande zote mbili.

Akiwahutubia wananchi waliokuwa wamefurika nje ya kituo cha Polisi cha Tunduma kufuatilia hatma ya sakata hilo, mkuu wa mkoa wa Mbeya, ambaye aliongoza ujumbe toka Tanzania, alisema kuwa mkutano baina yao ulikuwa wa mafanikio baada ya pande husika kukubaliana masharti waliyowekeana.

Alisema kuwa, katika mkutano huo yeye kwa niaba ya serikali ya Tanzania, aliwasilisha malalamiko mawili makubwa ambayo ujumbe wa Zambia uliyakubali nha kuahidi kuyafanyia kazi.

Aliyataja malalamiko hayo kuwa ni kupigwa risasi kwa raia wa Tanzania pamoja na kuuawa kwa mfanyibiashara Lucas Msuya, ambaye kifo chake ndicho kilisababisha machafyuko mpakani hapo.

Mkuu wa mkoa ambaye alikuwa ameambatana na Inspekta jenerali wa Polisi nchini, Bw. Said Mwema, alisema kuwa baada ya kuwasilisha malalamiko hayo, ujumbe wa Zambia ulikiri kuwepo kwa mapungufu yaliyosababisha hali hiyo, na kuahidi kulifanyia kazi tatizo hilo kwa kuanza kukichunguza kituo cha Polisi cha Nakonde.

Aliongeza kuwa, upande wa Zambia pia ulikubali kutuma wataalamu wake wa upasuaji kwa ajili ya kuja eneo la Nakonde kwa ajili ya kuufanyia uchunguzi mwili wa marehemu Msuya, ambaye inasadikika kuwa kifo chake kilitokana na mateso makali.

Ujumbe huo ambao utatoka katika jiji la Lusaka, utashirikiana na wataalamu kutoka serikali ya Tanzania, ambao wataongozwa na Bw. Robert Manumba, ambaye ni Mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai nchini.

Hata hivyo, mkuu wa mkoa aliongeza kuwa, licha ya kufikia makubaliano hayo, ujumbe wa Tanzania pia uliwaeleza wazi kuwa umechoshwa na vitendo vya uonevu ambavyo wamekuwa wakifanyiwa raia wake pindi wanapokuwa upande wa Zambia, na wakawatahadharisha kuwa ikiwa vitaendelea subira huenda ikawashinda Watanzania.

“Niliwaeleza wazi kuwa hali hii imetuchosha na kwamba ikiwa watarudia…….., mnajua” alisema mkuu wa mkoa huku akishangiliwa na maelfu ya wakazi waliokuwa eneo hilo.

Kwa upande wake Inspekta jenerali Mwema, akiongea na wananchi wa eneo hilo, alisema kuwa ujio wake ulikuwa ni kudhihirisha jinsi ambavyo serikali yao imekuwa ikiwajali, na akawashukuru sana kwa kufuata maelekezo ya mkuu wa mkoa pale alipowataka kuwa watulivu kwakuwa serikali inalifanyia kazi tatizo hilo.

“Wakazi wa Tunduma mmeonyesha jinsi gani Tanzania inastahili kuwa nchi ya kuigwa, uvumilivu, uelewa na subira yenu yamekuwa mambo ya muhimu sana katika kumaliza tatizo hili, na kwa niaba ya jeshi la Polisi na serikali kwa ujumla, nawaahidi kuwa matatizo kama haya yataendelea kudhibitiwa” alisema

Katika tamko hilo, serikali pia ilikanusha kuwepo kwa raia wa Tanzania waliiofanyiwa vitendo vya uonevu nchini Zambia, na ikaruhusu rasmi kufunguliwa kwa mpaka baina ya nchi hizi mbili, ambao jana ulikuwa umefungwa japo haikuwa rasmi.

Mara baada ya tamko hilo, wananchi waliokuwa wamefurika eneo hilo, walitawanyika huku wakiwa wanashangilia, na muda mfupi baadae makundi ya raia wa Zambia yalionekana yakivuka mpaka kuingia Tanzania kwa ajili ya kujipatia mahitaji yao, huku wakikaribishwa na Watanzania katika maeneo yao ya biashara.