Naam, Hii ndio Ari Mpya, Nguvu mpya na Kasi Mpya!, Haishangazi maana ukweli ni kuwa hatukuwahi kuelezwa kuwa ari hiyo, kasi hiyo na nguvu hiyo ni ya uelekeo gani na ndio maana kuna wakati nilihoji hilo ati.

Wakati CCM, ikiwa inatamba kila kona kuwa imempata mgombea ambaye ni kiboko na ‘Kiziba Mdomo’ cha wapinzani pia, imenishangaza sana kusikia kuwa jamaa huyu kipenzi cha watu ameutolea nje mdahalo uliokuwa umeandaliwa na kituo cha Televisheni cha Channel Ten.

Akiwa tayari ameshatuahidi kuwa ataendeleza yale yote mema yaliyoanzishwa na serikali ya awamu ya tatu ambayo kauli mbiu yake ilikuwa Uwazi na Ukweli, hakika jambo la kwanza kabisa ambalo tulilitarajia wengi wetu ni kuona anakuwa wazi zaidi ya aliyemtangulia, lakini hali imekuwa kinyume. Hali hii iwe ni kutokana na shinikizo la chama au kutoka kwake mwenyewe kwakweli haiwezi kupita hivi hivi kwasababu inazusha maswali mengi kichwani mwetu.

Je, Ni mangapi ambayo mhishimiwa huyu ataamua kuyatolea nje pindi akikanyaga pale kwenye lile jumba jeupe, na je hizi ni dalili za nini au kiashiria cha jambo gani kwetu Wadanganyika??

Naam, Mwendo mdundo, Ari Mpya, Kasi Mpya na Nguvu Mupyaaaaaaaaaaa!!!