Kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya Tanzania, mwaka huu wa 2005, ambako Tanzania inatarajiwa kufanya uchaguzi wake mkuu ambao utashirikisha vyama vingi vya kisiasa, vijana nchini humo wameamua kuwatolea uvivu waheshimiwa ambao wanatarajia kuzunguka mitaani siku chache zijazo kuanza kuwaomba Kura zao.

Wakiwa wanaunda sehemu kubwa ya Watanzania, (kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2002 vijana ni zaidi ya aslimia 65), vijana safari hii wameona kuwa haiwezekani wawape Kula jamaa zetu hawa, kwa kurubuniwa na peremende na makopo ya Juice. Wameamua kuhakikisha kuwa safari hii anapatikana kweli kiongozi au viongozi wa serikali ambayo itawajali hasa kwa kuwa wao ndio watakaokuwa sehemu kubwa ya kuwaingiza madarakani.

Katika kujiandaa na mchakato mzima wa kuhakikisha kuwa anapatikana kiongozi ambaye atakuwa mwenye kuvipa umuhimu vipaumbele vyao, vijana takriban 120, toka mikoa yote ya Tanzania wamekusanyika jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kile walichokiita Bunge Kivuli la Vijana wa Tanzania.

Pamoja na mambo mbalimbali, Bunge hilo ambalo kwa hakika utukufu wake ni wa uhalisia na wala sio wa ki-kivuli-kivuli kama walivyopenda kuliita, Vijana hao wameamua kujadili kwa kina juu ya mada kuu mbili ambazo zimekuwa zikiwaumiza sana kwa miaka nenda rudi sasa. Mada hizo ni Sheria ya mwaka 1971 kuhusiana na masuala ya Ndoa, pamoja na Sera ya Kitaifa ya Vijana.

Bunge hili limeandaliwa na taasisi ya vijana inayojulikana kwa jina la Youth of United Nations Association (YUNA), Tanzania, kwa ufadhili mkubwa wa shirika lisilo la kiserikali la kimataifa la African Youth Aliance (AYA)

Katika siku za karibuni nitawaletea hatua kwa hatua, msisimko na kila lililojiri ndani ya Bunge hili ambako nami kwa mara ya kwanza kabisa niliuonja Uhishimiwa, sijui haya ndio maandalizi kwa ajili ya kwenda kuwania jimbo la mtu au vipi. Haya tusubiri tuone.