Limekuwa ni jambo la kawaida sasa na wanachama wanaonekana sio tu kuikubali hali hii bali pia kuishabikia tena kwa nguvu zao zote zile walizonazo. Nazungumzia migogoro ndani ya vilabu mahasimu katika soka la Tanzania, yaani Simba na Yanga. Kwa hawa jamaa zetu, mafanikio ya soka ndani ya vilabu vyao ni mmoja kumfunga mwenzie, kama ambavyo kudorora kwa mmoja wao ni kufungwa na mwingine, hata iwe namna gani ikitokea hivi uongozi uliopo haunusuriki hata siku moja na kama huamini hebu soma hapa ujue yaliyojitokeza mtaa wa Jngwani (makao makuu ya Yanga), baada ya kufungwa 2-1 na Simba mwezi April mwaka huu.