Hata kama watu wataandamana kwa namna gani, bado haitosaidia kitu, ukweli utabakia pale pale kuwa tatizo la rushwa humu Duniani sio tu kwamba lipo bali pia linazidi kutukuzwa sana hasa na watawala wetu na haishangazi kuwa wamekuwa wakijitahidi sana kuihalalisha kwa kuipa majina mbalimbali kama hili Wadanganyika waliloambiwa ndio lenye kufaa sasa, TAKRIMA.

Ukiuliza kuna tofauti gani baina ya maneno haya, utaambiwa eti Takrima ni Bahshish na wala sio rushwa bali pale itakapokuwa imezidi, na ukiuliza kuwa kipimo cha kuijua kuwa imezidi kiasi cha sasa kuweza kuitwa rushwa kiko namna gani utaishia kuambiwa ‘ooh sijui kimepandia hapa kisha kikashukia kule, ooh sijui hili neno bwana lina asili ya kiarabu likimaanisha asante na mambo meeeeeengi yasiyo maana.

Imekuwa jambo la kawaida hivi sasa kuwa kujadili suala la Rushwa na mtu yeyote yule hasa awe kwenye hili kundi la hawa Watakavitu wetu, ni sawa na kupoteza muda wako bure maana utaishia kupigwa ngonjera za ajabu ajabu zisizo na kichwa, miguu wala kiwiliwili, utaishia kuambiwa mambo ambayo Watoto wa mitaa ya jiji la Dar es salaam hivi sasa wanakiita Longolongo, Lakini je ni kweli kuwa suala hili haliwezi kudhibitiwa kwa kiasi kikubwa japo kulimaliza kabisa imeshindikana??, huu ndio mjadala ambao napenda tushiriki kuujadili wanablogi wenzangu, karibuni