Amka mwanamke wa Kitanzania, amka mwanamke wa Kiafrika. Popote pale ulipo katika dunia hii, amka SAA YA UKOMBOZI NI SASA.Jitihada za mwanamke kutaka kujiondoa katika mfumo wa kukandamizwa kimawazo, kifikra, kimtizamo na kwa kila kitu ambacho amekuwa akidhania kuwa hakimstahili, hazijawahi kuwa na wakati mzuri kuliko sasa.

Harakati za kuhakikisha kuwa mwanamke kokote kule aliko duniani, anaendana na mazingira ya kisasa ya Utandawazi, Sayansi na Teknolojia, hususan katika eneo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEKNOHAMA) au (ICT) kama wanavyofupisha wenye lugha zao, zinatarajiwa kuchukua sura mpya hivi karibuni kufuatia mkutano mkubwa ambao utawakutanisha wanawake ambao wamekuwa wakitumia mfumo huo, kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Nauzungumzia mkutano ambao utawakutanisha wanawake ambao wamekuwa wakitumia teknolojia ya mtandao wa kompyuta katika kuwasiliana na kusambaza habari sehemu mbalimbali, mkutano ambao umepewa jina la BlogHer, ambao utafanyika nchini Marekani, mwezi Julai mwaka huu.

Mkutano huu pamoja na kuwa utakuwa fursa nzuri kwa wanawake kuweza kujadili mambo mbalimbali zikiwemo changamoto zinazowakabili wao wakiwa kama wanawake, katika ulimwengu wa sasa, pia unatarajia kuwa mkombozi wa wanawake wengi duniani ambao hawatoweza kubahatika kuhudhuria wenyewe, ambapo jitihada kadhaa tayari zinafanywa kwa ajili ya mambo yatakayozungumzwa na kujadiliwa huko, kuchapwa katika lugha mbalimbali, kikiwemo Kiswahili.

Je wewe ni mwanamke wa Kitanzania au wa Kiafrika ambaye unadhani kuwa teknolojia imekuwa ikikutupa nyuma kila unavyojitahidi kufuatana nayo?, Ulikosea, hebu kaa mkao wa kusubiri kujua kuwa wanawake wenzako wana ushauri gani kwako wewe ambao utaweza kukufanya nawe uende sambamba kabisa na kasi ya teknolojia hii ya mawasiliano na habari kwa njia ya mtandao wa kompyuta.

Unaweza kusoma maelezo zaidi kuhusu mkutano huo kwa lugha ya kiingereza kwa kuingia hapa, au hapa. Na kwa wale wenye kupenda kufuatilia katika lugha ya Kiswahili au lugha zinginezo, mnaweza kubonyeza hapa kwa ajili ya kujua nini kitakuwa kikitokea wakati tukielekea mkutano huo.

Amka mwanamke wa Kitanzania, Amka mwanamke wa Kiafrika, saa ya ukombozi wako ni sasa